SAUDI ARABIA: WAFANYAKAZI WA NYUMBANI AMBAO NI WAHAMIAJI KATIKA NCHI ZA NJE HUPITIA UNYANYASAJI, UBAGUZI WA RANGI NA HAWALINDWI NA SHERIA ZA KAZI

Wanawake wa Kenya ambao huajiriwa kufanya kazi za nyumbani Saudi Arabia hulazimika kuvumilia mazingira ya kazi ambayo ni ya kikatili na kibaguzi. Mazingira haya yanaweza kufananishwa na kazi ya kulazimishwa na ulanguzi wa watu, Amnesty International imesema katika ripoti yake. Ripoti hiyo inaangazia namna waajiri wanavyowanyanyasa wanawake hawa majumbani mwao kutokana na mitazamo ya ubaguzi wa rangi, na namna wafanyakazi wa nyumbani wanavyotengwa na sheria ya kazi na mageuzi yanayohusiana na kazi nchini Saudi Arabia.

Wamefungiwa ndani, Wametengwa:  Maisha yaliyofichwa ya wafanyakazi wa nyumbani kutoka Kenya wanaofanya kazi nchini Saudi Arabia, inafafanua mambo waliyoyapitia zaidi ya wanawake 70 ambao waliwahi kufanya kazi nchini Saudi Arabia. Mara nyingi wanaowatafutia kazi wanawake hawa huwadanganya kuhusu hali ya kazi watakazofanya lakini wanapofika Saudi Arabia wanalalazimika kufanya kazi katika mazingira magumu sana. Wakati mwingine wanafanya kazi kwa zaidi ya masaa 16, wananyimwa siku ya mapumziko na kuzuiwa kutoka  nje ya nyumba. Wanawake hawa pia huishi katika mazingira yasiyo na utu kabisa. Wengine wanabakwa, wanatukanwa na kupigwa.  Waajiri walichukua pasipoti na simu zao na wakati mwingine walikataa kuwalipa mishahara.

Wanawake hawa walienda Saudi Arabia kutafuta kazi ili wasaidie familia zao lakini wakajipata wakivumilia mateso makali majumbani mwa waajiri wao. Serikali ya Kenya inawahimiza raia wake kutafuta kazi nje ya nchi nayo mamlaka ya Saudi Arabia wanadai kwamba wameanzisha mageuzi kuhusu haki za ajira. Hata hivyo majumbani mwa waajiri, wanawake wanaendelea kukabiliwa na ubaguzi wa rangi, mateso na unyanyasaji wa hali ya juu sana.

Irungu Houghton, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Amnesty International nchini Kenya

Mamlaka za Kenya na Saudi Arabia lazima ziwasikilize wanawake hawa; ambao kazi yao ndiyo inayodumisha familia na kuchangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi hizi mbili. Kwa dharura, mamlaka za Saudi Arabia zinapaswa kuwapa wanawake hawa ulinzi chini ya sheria ya kazi, waanzishe mfumo mzuri wa kufanya ukaguzi ili kukabiliana na mateso yanaoendelea kwenye nyumba za waajiri wa kibinafsi. Pia wavujilie mbali kabisa mfumo wa kafala ambao huwaweka wafanyakazi chini ya udhibiti wa waajiri wao, unakuza unyanyasaji na ubaguzi wa kimfumo.

Irungu Houghton, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Amnesty International nchini Kenya

Hakuna kati ya mamlaka za Kenya na za Saudi aliyejibu Amnesty International ilipowaomba kutoa maoni au taarifa.

Hii ilinifanya nihisi kana kwamba ni gereza

Kazi nyingi kupindukia lilikuwa tatizo kwa wanawake wengi ambao walizungumza na Amnesty International, huku kwa kawaida wakifanya kazi kwa masaa 16, na mara kadhaa, kwa masaa hata zaidi. Kazi hizi ni pamoja na kusafisha, kupika na kuwatunza watoto. Walilipwa wastani wa SAR 900 (USD 240) kwa mwezi, na hakuna aliyelipwa kwa kazi ya ziada, kumaanisha wastani wa mshahara wao ukizingatia masaa waliyofanya kazi ulikuwa USD 0.5 kwa saa. Zaidi ya hayo, baadhi ya waajiri walichelewesha mishahara au hawakulipa chochote. Takribani wanawake wote waliohojiwa walisema kwamba hawakuwahi kupewa siku ya mapumziko wakati huo wote waliofanya kazi Saudi Arabia – wengine wakiwa pale kwa hadi miaka miwili.

Hakuamini (mwajiri) kwamba ninaweza kuchoka. Hakukuwa na nafasi ya kupumzika… Ningemfanyia kazi mchana kucha na hata usiku, bado ningekuwa nikifanya kazi. Nilijihisi kama punda ingawa hata punda hupata kupumzika.

Rashida*, aliyewahi kuwa mfanyakazi wa nyumbani

Wanawake wote walisema kwamba walikabiliwa na vizuizi vya uhuru na usiri wao; kutwaliwa kwa simu zao kuliwafanya wasiweze kuzungumza na watu wa nje, hivyo wakajihisi kutengwa sana na pia kunyimwa nafasi ya kuwasiliana na familia zao.

Joy* alisimulia kuhusu namna alivyojihisi kama mtu aliyenaswa kwenye mtego wakati akiwa Saudi Arabia.

Sina uhuru wowote kwa sababu unapoingia, huwezi kutoka. Hutoki wala huoni nje.” Hii ilinifanya nihisi kana kwamba ni gereza

Joy*, aliyewahi kuwa mfanyakazi wa nyumbani

Eve*, aliongezea kwa kusema kwamba kufungiwa huku kulitumika kumzuia asilalamike kuhusu hali yake.

Jambo la kwanza aliliofanya bosi wangu ni kuchukua pasipoti yangu. Ukiulizia, watakwambia ‘nimekulipia kila kitu… na huwezi kuthubutu kusema jambo lolote kwa sababu uko ugenini

Eve*, aliyewahi kuwa mfanyakazi wa nyumbani

Kando na kazi nyingi kupindukia, takribani wanawake wote walisema kwamba waajiri wao waliwanyima chakula au waliwapa mabaki, hivyo kuwafanya baadhi yao kuishi kwa mkate au noodles. Katherine* alisema kwamba “tatizo kubwa ilikuwa chakula”  Alieleza kuwa mwajiri wake alimpatia tu mabaki ya chakula, chakula kilichooza, au wakati mwingine hakumpatia chochote kabisa. Katherine alisimulia kuwa alipojaribu kupika chakula chake mwenyewe, mwajiri wake alimpigia kelele na kukitupa kwenye pipa akisema kinanuka. Kwa sababu hiyo, Katherine alisema aliishi kwa kula biskuti tu.

Wanawake wengi pia walielezea kwamba hali ya maisha ilikuwa duni sana, mara nyingi walilazimika kulala kwenye stoo, au sakafuni kwenye chumba cha watoto, na bila kitanda kizuri, matandiko wala kiyoyozi cha kupunguza joto chumbani.

Mume (wa nyumba) alisema ‘utafanya nitakachotaka’

Wanawake wengi walikumbuka jinsi walivyokemewa, kutukanwa na kudhalilishwa huku wengine wakifanyiwa ukatili wa kingono na baadhi yao walibakwa na waajiri wao wa kiume. Hii ni pamoja na Judy, mama wa watoto wawili ambaye alikuwa ameenda Saudi Arabia ili kukimbia mumewe aliyekuwa akimdhulumu.

Alinibaka na hata akanitishia nisimwambie mkewe. Nilinyamaza. Alinifanyia haya karibu kila siku… Nilijaribu [kumwambia akome] lakini wanaume wana nguvu sana. Kwa hivyo alinibaka, mara tano…

Huku wengi wakiwa na hofu sana kuripoti unyanyasaji waliopitia kwa mamlaka za Saudi au ubalozi wa Kenya, waliothubutu kufanya hivyo waliishia kulipiziwa kisasi au kusingiziwa makosa kama vile ya wizi na hivyo kupoteza mishahara yao.

Walituita nyani au sokwe

Ripoti pia inaangazia jinsi ubaguzi wa kimfumo wa rangi uliojikita ndani ya mfumo wa kafala, pamoja na mitazamo ya kibaguzi iliyozama kutokana na historia ya utumwa na ukoloni wa Waingereza katika eneo hilo. Pia inaonyesha jinsi mambo haya yanavyoendeleza unyonyaji, unayasaji na ubaguzi wa rangi dhidi ya wafanyakazi hawa — hasa wanawake — ambao hali yao ya kuwa wafanyakazi wa nyumbani wahamiaji huwafanya kuwa katika mazingira hatarishi.

Wanawake wengi walieleza jinsi waajiri wao waliwaita kwa majina ya kudhalilisha na ya kuwabagua kirangi, kwa mfano  “hayawani” (mnyama), “khaddama” (mtumishi) na “sharmouta” (kahaba).  Waajiri pia wangetoa maneno ya dharau kuhusu rangi ya ngozi ya wafanyakazi, walitoa maoni kuhusu harufu ya miili yao, au kuwazuia kutumia vyombo vya jikoni au vifaa vingine vya nyumbani vinavyotumiwa na familia — jambo ambalo wanawake hawa walilitaja mara nyingi kama “kutengwa” — kwa sababu walitoka Afrika.

Kwa sababu ya rangi yangu nyeusi, kila mara waliniita mnyama Mweusi. Watoto pia wangekuja kwa uso wangu na kuninyooshea kidole wakisema namna ninavyofanana na nyani.

Niah* aliyewahi kuwa mfanyakazi wa nyumbani

Kiini cha unyanyasaji huu ni mfumo wa ajira unaoendeshwa na ubaguzi wa rangi wa kihistoria na kimfumo, ambapo wafanyakazi wa nyumbani kutoka nje — hasa wanawake weusi kutoka Afrika — wanatendewa kinyama kana kwamba hawana thamani wala utu.

Irungu Houghton, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Amnesty International nchini Kenya

Sheria na mageuzi yasiyotosha

Katika miaka ya hivi karibuni, kama sehemu ya mpango wake wa Dira ya mwaka 2030, Saudi Arabia imeanzisha mageuzi machache katika mfumo wa kafala unaowaweka wafanyakazi wahamiaji milioni 13 wa nchi hiyo chini ya udhibiti wa waajiri wao na ambao unachangia moja kwa moja kuwepo kwa kazi ya kulazimishwa na ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu.

Licha ya mageuzi haya machache yanayohusisha zaidi wafanyakazi wanaolindwa na sheria ya kazi ya Saudi Arabia, wafanyakazi wa nyumbani bado wanatengwa. Hadi waleo, wafanyakazi wa nyumbani bado wanawekewa masharti makali kuhusu uhuru wao wa kusafiri, na mara nyingi bado watahitaji ruhusa ya mwajiri wao ili kubadilisha kazi au kuondoka nchini.

Mnamo 2023, serikali ilianzisha Kanuni mpya za Wafanyakazi wa Nyumbani ili kudhibiti vyema masaa na mazingira ya kazi. Hata hivyo, bila mfumo mzuri wa ufuatiliaji, ukaguzi na utekelezaji mzuri wa sheria, kanuni hizi mara nyingi huwa hazina maana yoyote kiutendaji. Visa vingi vya unyanyasaji vilivyorekodiwa ni kinyume cha sheria za Saudi Arabia lakini bado ulitendwa kwa kutokujali kamwe.  

Kenya ina jukumu kubwa katika kulinda wafanyakazi wa nyumbani wanaofanya kazi ughaibuni. Inapaswa kushirikiana na Saudi Arabia kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji kwa kudhibiti vyema taratibu za kazi na kuhakikisha ubalozi una vifaa na uwezo wa kuwasaidia kwa dharura wafanyakazi wa nyumbani walioko katika hatari, ikiwa ni pamoja na kuwapatia hifadhi salama pamoja na msaada wa kifedha na wa kisheria kwa wale wanaohitaji

Irungu Houghton, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Amnesty International nchini Kenya

*Majina yamebadilishwa

Usuli

Takriban watu milioni 4 wanafanya kazi za nyumbani nchini Saudi Arabia, wote wakiwa ni raia wa kigeni kulingana na takwimu za soko la ajira za nchini humo. Miongoni mwao ni Wakenya 150,000. Kutokana na kiwango cha juu cha ukosefu wa kazi nchini Kenya, maafisa wa serikali wamekuwa wakihimiza vijana kutafuta kazi katika nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ikiwemo Saudi Arabia, ambayo ni mojawapo ya nchi ambazo huletea Kenya fedha kutoka kwa raia waishio ughaibuni. 

Ili kupata taarifa zaidi au kupanga mahojiano, wasiliana na:

Nchini Kenya:

Wasiliana na Mathias T. Kinyoda Mobile: +254723424802 | Barua pepe: [email protected] 

Kimataifa:

Email: [email protected], T: +44 (0)7472681674