WAMEFUNGIWA, WAMETENGWA: MAISHA YALIYOFICHWA YA WAFANYIKAZI WA NYUMBANI KUTOKA KENYA WANAOFANYA KAZI NCHINI SAUDI ARABIA

Ukiwa katika nchi kama Saudi Arabia, huna pesa, uko peke yako kwa hivyo huna msaada wowote… Nilikuwa nimefungiwa ndani, kutoka nje haikuruhusiwa. Sijawahi kutoka nje ya nyumba na sikuwahi kuwa na siku ya mapumziko.

Hope*, ambaye alirejea Kenya baada ya kufanya kazi kama mfanyakazi wa ndani nchini Saudi Arabia

Historia

Saudi Arabia ni makao ya takriban wafanyakazi wa ndani milioni 4, wakiwemo wanawake milioni 1.2 na wanaume milioni 2.7 kutoka Afrika na Asia ambao wana mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo na katika kusaidia maisha ya kifamilia. Hata hivyo, uzoefu wa wanawake wa Kenya ulioelezwa katika ripoti hii unaonesha jinsi wafanyakazi hawa wanavyokumbana na mazingira magumu, ya kikatili na ya kibaguzi kazini, hali ambazo mara nyingi hufikia viwango vya ajira ya kulazimishwa na usafirishaji haramu wa binadamu.

Wajiri haramu waliwauzia wanawake walihojiwa katika ripoti hii ndoto ya maisha bora kabla ya kuwatumbukiza katika hali ya mateso makubwa, upweke na unyanyasaji mkubwa katika nyumba za watu binafsi. Walitumia shinikizo za kiuchumi zinazoathiri maisha ya wanawake na kuwatatiza katika kufanya maamuzi — ukosefu mkubwa wa ajira, fursa chache hapa nchini Kenya, na majukumu ya kulea na kusomesha watoto. Walipowasili Saudi Arabia, mara kwa mara walilazimishwa kufanya kazi kwa zaidi ya saa 16 kwa siku bila mapumziko, na mara nyingi bila siku hata moja ya kupumzika kwa miezi au hata miaka. Wengine hawakuruhusiwa kamwe kutoka nje ya nyumba, na wengi wao walikatwa kabisa mawasiliano na ulimwengu wa nje. Katika maeneo yao ya kazi, ambayo pia yalikuwa makazi yao, hapakuwa na njia ya kuepuka matusi, kudhalilishwa, ubaguzi wa rangi, na unyonyaji wa hali ya juu. Katika visa vingi, walipigwa au kudhulumiwa kingono. Baadhi yao walibakwa na waajiri wao wa kiume au watoto wa waajiri hao. Wengi wao walikumbwa na kucheleweshwa kwa malipo au kutolipwa kabisa mishahara yao midogo. Karibu wote walinyang’anywa pasi zao za kusafiria walipowasili, jambo lililowafanya kushindwa kutoroka waajiri wakatili, ambao hawakuchukuliwa hatua zozote za kisheria.

Athari za jumla za uzoefu huu ziliwaacha wanawake hawa na majeraha ya kina ya kimwili na kiakili. Baadhi yao hadi leo wanakumbwa na matatizo sugu ya kiafya na msongo wa mawazo uliotokana na mateso waliyoyapitia Saudi Arabia.

Ripoti hii inategemea mahojiano ya kina yaliyofanywa ana kwa ana mwaka wa 2024 na wanawake 72 Wakenya waliorejea hivi majuzi kutoka Saudi Arabia, waliokuwa wakisaidiwa na mashirika kutokana na ukatili walioupitia. Pia inajumuisha mazungumzo na mashirika ya kiraia nchini Kenya, uchambuzi wa mfumo wa kisheria wa Saudi Arabia, fasihi kuhusu biashara ya utumwa ya Afrika Mashariki na athari zake, na tathmini ya ripoti kutoka kwa taasisi za Umoja wa Mataifa, Shirika la Kazi Duniani (ILO), na mashirika ya kimataifa, kikanda na kitaifa yasiyo ya kiserikali. Amnesty International iliwaandikia mamlaka za Saudi Arabia ikiomba taarifa kuhusu sheria na mageuzi ya hivi karibuni, lakini haikupata majibu. Shirika hilo lilikutana na maafisa wa Kenya mnamo Machi 2024 kujadili matokeo ya awali ya utafiti, lakini pia halikupokea majibu ya maombi ya maandishi yaliyofuata.

Ingawa ripoti hii haitoi madai kuwa kila mfanyakazi wa ndani nchini Saudi Arabia anakumbwa na mazingira magumu kazini, wala kwamba kila mwajiri ni mkatili, inafichua mifumo ya ukatili mkubwa unaochochewa na mfumo wa uhamiaji na ajira unaotoa mamlaka makubwa kwa waajiri dhidi ya wanawake wanaofanya kazi katika nyumba binafsi, huku ukiwanyima njia halisi za kujinasua kutoka katika mazingira hatarishi na kuwawajibisha waajiri wakatili.

Wanawake wengi waliohojiwa na Amnesty International walihamia Saudi Arabia kutokana na matatizo ya kiuchumi na hitaji la kusaidia familia. Kwa kuwa karibu asilimia 40 ya Wakenya waliishi chini ya mstari wa umaskini mwaka wa 2022, serikali imekuwa ikihamasisha vijana kutafuta ajira nje ya nchi kama suluhisho kwa ukosefu mkubwa wa ajira. Kati ya 2020 na 2022, fedha zinazotumwa kutoka Saudi Arabia ziliongezeka zaidi ya mara mbili, na maafisa wa Kenya wanakadiria kuwa kuna hadi Wakenya 200,000 wanaoishi huko kwa njia ya kawaida ya uhamiaji, wakiwemo zaidi ya wafanyakazi wa ndani 150,000, wengi wao wakiwa wanawake.

Ukatili mkubwa — na katika visa vingi wa kihalifu — walioupitia wanawake waliohojiwa katika ripoti hii unasababishwa na mambo kadhaa. Kwanza, licha ya mabadiliko madogo katika mfumo wa udhamini wa kafala — mfumo wa ajira unaowafunga wafanyakazi wa kigeni kwa waajiri wao kama wadhamini rasmi — bado unaendelea kuwateka wafanyakazi wa ndani, kuwafanya wategemee waajiri wao kwa kila nyanja ya maisha yao, na kuwanyima uwezo wa kubadilisha ajira au kuondoka nchini bila ruhusa ya mwajiri. Pili, unyanyasaji huu unachochewa na kutotambuliwa kwa wafanyakazi wa ndani katika Sheria ya Kazi ya Saudi Arabia, hali inayowafanya wafanyakazi walioko katika mazingira hatarishi zaidi kuwa na ulinzi hafifu zaidi ikilinganishwa na sekta nyingine. Tatu, ukosefu wa mifumo thabiti ya kutekeleza sheria na udhaifu wa mageuzi ya hivi karibuni ya kazi unazidisha hali hiyo. Hatimaye, haya yote yanaimarishwa na ubaguzi wa kimfumo unaoendelea kuwepo Saudi Arabia, ukiwemo mfumo wa kibaguzi unaoendelezwa na kafala na mitazamo ya kijamii iliyojaa ubaguzi wa rangi.