Ubaguzi ndio Tisho Kubwa kwa Familia za Kenya

Familia ni kiungo muhimu sana katika kila jamii. Hapa Kenya hili limetambulika wazi katika sheria kuu ukurasa wa 4, kipengee cha 45. Kando na yaliochapishwa kisheria familia ziko aina nyingi kulingana na jamii na maelewano ya wanaohusiana kifamilia.

Kuna mengi yanayokumba familia ambayao athari zake zinafikia jamii nzima kwa njia tofauti ikiwemo ubaguzi. Ubaguzi hujitokeza ki aina tofauti iwe kwa maneno au vitendo, kwa mfano kutengwa, kunyanyaswa, kulengwa kwa unyanyapaa, na dhulma zinginezo ambazo ni vigumu kutambulika isipokua kwa aliye makini.Tukumbuke kua ubaguzi ni kinyume cha makubaliano, kwa  mfano Taarifa ya Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu kifungu cha kwanza kinachosimulia kua “Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa,”  na sheria kuu ya Kenya, ukurasa wa 4, kipengee cha 27, inayohakikishia wakenya usawa na uhuru kutokana na ubaguzi. Kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty International Kenya 2023 (Is Article 27 Under Attack?), kati ya watu 2, 1 anapitia ubaguzi wa aina flani, takwimu hizi ni za kutamausha na inaashiria tatizo kubwa zaidi katika jamii yetu ya Kenya, kitovu chake ikiwa familia.

Mara nyingi, wazazi wamelaumiwa kuanza ubaguzi wa wana wao tangu utotoni, lakini sio rahisi kutambulika hadi pale watoto hao aitha wanabalehe ama wanakomaa na kuelewa yalio wakumba tangu utotoni. Inchini Kenya, kati ya yale yamesemekana kua vyanzo vya ubaguzi ni kama yafwatayo: Jinsi ya kupeana majina kwa watoto, ulemavu, jinsia, hali ya utasa, uwezo wa kifedha, uerevu wa mtu, tabia ya mtu, ukabila, dini na mengineo. Nakala hii inaangazia familia kwa muktadha wa Africa na haswa Kenya, inajaribu kudadavua  vyanzo vya ubaguzi ndani ya familia, hatari yake kwa ushirikiano na mapenzi katika familia na ni vipi athari zake zinayumbisha uwiano katika jamii nzima ya wakenya.

Tukiangazia hali ya ulemavu, watoto wengi walio na ulemavu wamejipata wanyonge maishani sababu ya kunyimwa haki za kimsingi ikiwemo chakula bora, mavazi, makao bora na mengineo. Unyanyapaa unaoshuhudiwa kwa walio na ulemavu umechangia pakubwa watoto walemavu kufichwa majumbani huku wazazi wakihofia aibu na masengenyo yanayofuatia hali hio. Hivyo basi, watoto hao huzidi kupitia madhila yasio kifani kwa mtazamo wa jamii iliyojaa dhulma, unyanyapaa na ufidhuli, huku maisha yao yote yakiharibika tu, kwa ajili ya maumbile yao. Aila kadha wa kadha nchini zinapitia hali hio sio tu kwa walemavu lakini pia kwa vitambulisho vyingine vya binadamu kama tunazoangazia katika nakala hii.

Familia nyingi hivi sasa, zina watoto ambao sio wa mzazi mmoja kati ya wale wanandoa na hii inaweza kua kwa maelewano yao au kwa kisa kilichotokea hapo awali ambapo mmoja alijipata na mtoto/watoto. Watoto kama hawa pia hubandikwa majina (wanaharamu), na wengine hupitia dhulma za kingono na kijinsia kutoka kwa mzazi mmoja huku wakitahadharishwa na kuripoti. Sio wengi wanaofanikiwa kuepuka madhila haya na hivyo basi hubeba machungu yao bila msaada wowote.

Kijinsia, tamaduni imekua kutambua jinsia mbili ila sasa kuna aina tofauti na kati ya hayo ya tatu iliotambulika kisheria ni huntha. Desturi za jamii nyingi inchini zimenenzi sana kua na watoto wa jinsia ya kiume kama vifungua mimba. Kwa wale walio shika tamaduni hio sana husikitika wanapojua kua kifungua mimba wao sio wa kiume ila ni huntha au wa kike. Jambo hili limechangia hadi ndoa kuvunjika kwa tuhuma potovu za kua mke ana laana au alifanya usherati ili kutokea hali hio.

Uwezo wa kifedha umeonekana kuchangia ubaguzi haswa kwa wale wasio na uwezo ndani ya familia nyingi. Kwa mfano wakati wa mipango ya kijamii kama harusi au mazishi, wanaosikilizwa na kua na usemi mkubwa ndani ya boma ni wale walio na uwezo mkubwa kifedha. Jambo hili hutenganisha familia kwa kiasi kikubwa na kufanya wengine kujiona kama hawafai. Kwa jamii zingine, vile mtu anavyozikwa pia ni ishara ya uwezo wake aliokua nao akiwa hai. Walalahoi huzikwa na watu kidogo kulinganisha na matajiri ndani ya jamii hio moja.

Kwa bahati mbaya, wanawake ndio hubeba mzigo mkubwa katika familia ikija kwa maswala ya ubaguzi. Mwanamke anapojifungua tuhuma tofauti kutokana na watoto huelekezwa kwake pindi tuliyoyajadili hapo juu hutokea. Upande mwingine, ikiwa mwanamke huyu hana uwezo wa kujifungua pia hupitia unyanyapaa na matusi na pia huenda akaachika huku akiitwa tasa. Muhimu kutambua kua imedhibitishwa kua, hali ya utasa unaathiri wake kwa waume. Wanawake wa aina hii huenda wakapitia dhulma aina nyingi hadi uzeeni kwa kutengwa na kukosa wa kumshughulikia mahitaji yake haswa akiwa mtalaka au mjane, mgonjwa, mlemavu, fukara mtawalia. Kwa wanawake waoachwa kwa ndoa au kwa sababu zingine akajipata kua ndiye mlezi wa pekee, jamii imeonesha ukatili kwa njia nyingi huku wakipewa majina yakuwashusha hadhi na kuwanyima nafasi za ajira, uongozi na hata kuwatusi hadi mitandaoni pasi na kuelewa changamoto wanazopitia.

Familia zilizoko na watu wasio kabila moja na pengine dini moja pia hupitia changamoto nyingi amabazo huisambaratisha. Kwa ukabila haswa siasa zinapochacha wengi hukimbilia kwa jamii zao lakini kwa walio na mchanganyiko wa kabila mara nyingi jamii zao huwakataa wakisema wao sio jamii fulani kamili hivyo basi hawana haki za kitanaduni. Hali hii imechangia kua na wale wasiotaka kutangamana na jamii zao wakihofia kutengwa.

Wanasaikolojia wametambua kua tabia huathirika na mambo mengi yakiwemo yale binadamu aliyopitia utotoni. Ubaguzi nao umedaiwa kuleta madhara makubwa kama watu kujitoa uhai, uhalifu, na kudorora kwa hali ya maisha ya jamii.

Kwa ufupi ubaguzi katika familia ni chanzo cha ubaguzi katika jamii na iwapo suluhu ya kudumu itapatikana basi mwanzo wake lazima iwe katika familia. Tofauti za kimaumbile mafikira, tamaduni au hata imani ni lazima tuzikubali kama mchango wetu katika ulimwengu na tubadilishe mtazamo wetu kwa wengine, muhimu kua wao ni binadamu wenye haki sawa kama wengine.

Zaina Kombo is Amnesty International Kenya Equality and Anti-Discrimination Campaign Manager and writes in her personal capacity. Email: [email protected]